Friday, February 22, 2013

at Wednesday, February 20, 2013 WATAHINIWA KIDATO CHA NNE WACHORA KATUNI KATIKA KARATASI ZA KUJIBIA MTIHANI Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Joyce Ndalichako akionyesha karatasi ya majibu ya mmoja wa watahiniwa wa mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2012, Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi Fredy Azzah, Joyce Mmasi WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inaweza kukumbwa na kashfa kubwa kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne ya 2012 yaliyotangazwa juzi na Waziri wake, Dk Shukuru Kawambwa. Kashfa hiyo inatokana na aina ya majibu yaliyoandikwa na baadhi ya watahiniwa katika mitihani hiyo, huku wengine wakikusanya vitabu vya majibu bila kujibu chochote, hali inayohusishwa na uhaba mkubwa wa walimu katika baadhi ya shule za sekondari nchini. Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta), Dk Joyce Ndalichako alisema wasahihishaji walikutana na mambo ya ajabu yakiwamo matusi, michoro ya vitu visivyoeleweka, mashairi na nyimbo za muziki wa kizazi kipya (bongo fleva). “Mwaka jana tulikutana na ‘single’ yaani waliandika mashairi kwa uchache, lakini mwaka huu tumepata albamu nzima… ni vituko vitupu, wengine wanaandika mapenzi, mwanafunzi anatumia ukurasa mzima kumlalamikia mpenzi wake. Miongoni mwa yaliyoandikwa ni mpenzi, umeniacha, natamani kunywa sumu, usiku silali nakuwaza wewe…” alisema Dk Ndalichako. Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili ofisini kwake Dar es Salaam jana, Dk Ndalichako alisema wanafunzi wengine waliandika malalamiko dhidi ya wabunge na uendeshaji wa Bunge. “Unakuta mwanafunzi anaeleza anavyolishangaa Bunge… mtu anaandika… nawashangaa wabunge, wamekaa kama wapo kijiweni, wabunge wamekosa ustaarabu, badala kujadili kero za wananchi waliowachagua, wanapokea timu zilizoshinda makombe… timu ikishinda Kombe la Kagame inapokelewa bungeni. Bunge limekuwa kama kijiwe, bungeni siyo ukumbi wa starehe kama mnataka kupokea timu hizo nendeni katika ofisi zao au viwanjani…” alisema. Alisema wanafunzi walioandika vitu visivyoeleweka walikuwa ni wengi na walichangia kwa kiasi kikubwa matokeo kuwa mabaya. Dk Ndalichako alionyesha baadhi ya michoro hiyo ambayo inaonyesha vikaragosi ambavyo wanafunzi hao waliviita Messi (Lionel, mchezaji wa Barcelona) na zombi (ni picha za kutisha) ambazo huonyeshwa kwenye televisheni. Sababu za kufeli Dk Ndalichako alisema hawezi kuwa na jibu la moja kwa moja juu ya kwa nini matokeo ya mwaka huu yamekuwa mabaya, lakini akadokeza kuwa huenda yametokana na wanafunzi wengi kukosa maarifa. Anasema mbali na waliojaza matusi na michoro, wanafunzi wengine waliofanya vibaya ni wale ambao hawakujaza chochote kwenye karatasi zao za majibu. “Kuna baadhi ya shule unakuta darasa zima watoto hawajajibu somo fulani kwa mfano Biolojia, wanaingia tu na kuandika namba. Tuliamua kuwapigia simu walimu wao, majibu waliyokuwa wakitupa ni kuwa hawajawahi kuwa na walimu wa somo husika kwa hiyo watoto hawakuwa na cha kujaza.” Dk Ndalichako alisema kwa ku mbukumbu zake, hakuna matokeo mabaya kama ilivyo kwa mwaka huu yaliyowahi kutokea. “Tukiangalia tu kuanzia 2000, hakujawahi kutokea matokeo mabaya kama haya, kwa kweli hali haipendezi. Hata kabla ya kuyatangaza nilikuwa nayaangalia mara tatu tatu, sikuyapenda na inasikitisha kwa kweli,” alisema Dk Ndalichako. Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment