Mgogoro
ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umeingia katika
sura mpya baada ya viongozi wake wawili waandamizi, Naibu Katibu Mkuu,
Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo kuuandikia uongozi
wa chama hicho wakitaka uikane taarifa inayowachafua mitandaoni.
Zitto
na Dk Mkumbo wanatuhumiwa kupokea fedha na kushirikiana na viongozi wa
Idara ya Usalama wa Taifa na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nia
ya kuivuruga Chadema.
Taarifa hiyo
yenye kichwa cha habari 'Ripoti ya siri juu ya Zitto Kabwe’, ambayo
imesambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii katika siku za karibuni
inadaiwa kuwa iliandaliwa na Kitengo cha Upelelezi cha Chadema baada ya
uchunguzi wa mwenendo wa Zitto ndani na nje ya nchi kuanzia mwaka 2008.
Sehemu
ya taarifa hiyo ya mtandaoni inadai kuwa Zitto alipelekewa kiasi cha
Dola za Marekani 266,000 (Sh416 milioni) huko Ujerumani na maofisa wa
Usalama wa Tanzania, Desemba 16, 2009.
Ripoti
hiyo inadai kuwa fedha hizo zilipitishwa katika Benki ya Berliner ya
Ujerumani kwenye akaunti ya raia wa nchi hiyo, Andrea Cordes, ambaye
anadaiwa kumpelelekea Zitto.
Taarifa zaidi zinadai kuwa fedha hizo ziligawiwa kwa wafuasi mbalimbali wa chama hicho na miongoni mwao ni Dk Mkumbo.
Zitto amlima barua Dk Slaa
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Zitto alisema amemwandikia
barua Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa kumwomba athibitishe
‘Taarifa ya Siri ya Chadema’ kama ni ya kweli au chama hicho kiikanushe
ili aweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa kile
alichokiita ‘hekaya.’
“Taarifa
ya Chadema inasema kwamba chama hicho (chama changu), kilikuwa
kimechunguza mwenendo wangu tangu mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini kuwa
mimi ninapokea fedha kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga
Chadema,” alisema Zitto kwenye taarifa yake.
Zitto alisema taarifa
hiyo ni ya kutunga na iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha,
imemfedhehesha, imemsikitisha na kumkasirisha.
Alisema
taarifa hiyo iliibuliwa katika kipindi ambacho alikuwa ziarani barani
Ulaya katika nchi za Uswisi na Uingereza ambako alikuwa anafuatilia
fedha zilizofichwa na Watanzania katika nchi hizo.
“Pengine
lengo la ripoti hiyo lilikuwa ni kutaka kunipoteza kutoka katika nia na
dhamira yangu ya dhati ya kutaka Watanzania wafaidike na utajiri wao.
Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo waliamua kutoa taarifa yao unazua
maswali mengi kuliko majibu,” alieleza Zitto katika taarifa yake.
Dk Mkumbo alia na uenezi
Dk Mkumbo alieleza kusikitishwa na Idara ya Uenezi ya Chadema kwa kukaa kimya bila kutoa maelezo juu ya suala hilo.
“Hasa
pale ambapo tumeambiwa waraka huu umetoka makao makuu. Hii si kawaida
kwa idara yetu hii nyeti iliyosheheni watu mahiri. Mara zote huwa wepesi
kabisa kwa vijana wetu katika idara hii kutoa ufafanuzi, tena kwa mambo
mepesi kabisa yanayokigusa chama, vipi makamanda kwenye jambo hili
imekuwaje?” aliandika Dk Mkumbo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa
Facebook jana na kuthibitisha kwa simu.
Dk Kitila alisema pamoja na umaskini wake, hajawahi kuhongwa popote na wala hatarajii.
“Taarifa
zinazosambazwa kuhusu mimi ni za uongo wa kijinga na uzushi wa kitoto
kwa malengo ya siasa nyepesi. Ni wazi kwamba wanaosambaza habari chafu
kunihusu hawanijui na ndiyo maana wanaweza kudiriki kuzusha kwamba mimi
Kitila Mkumbo naweza kuhongwa Sh200,000.”
Alihoji
pia Chadema ilikuwa na siri gani za hatari kiasi cha kumfanya Zitto,
ambaye ni rafiki yake wa siku nyingi kuhongwa kiasi hicho kikubwa cha
fedha.
Mnyika awajibu
Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa Chadema, John Mnyika ameikana ripoti hiyo na kueleza kuwa haijaandikwa na makao makuu ya Chadema.
Mnyika alisema Zitto ameibua kitu ambacho anafahamu kuwa kimeshughulikiwa na uongozi wa chama hicho.
“Zitto
anajua kuwa Andrea Cordes aliniandikia baruapepe na nakala kwake
nikawajibu kuwa ripoti hiyo haijaandikwa na Makao Makuu ya chama na
tukipokea malalamiko rasmi tutachunguza kwa sasa chama kinaichukulia
ripoti hiyo kama ripoti nyingine zinazosambazwa mitandaoni,” alifafanua
Mnyika.
Akizungumzia malalamiko ya Dk Mkumbo, Mnyika alisema alikuwa anapaswa kufuata taratibu za chama kama alikuwa na malalamiko.
Alisema
baada ya taarifa hiyo ya siri kusambaa mtandaoni, Zitto alitoa kauli na
kama Dk Mkumbo hakuridhika, alipaswa kuonana na watu wa Idara ya Uenezi
ya Chadema.
“Idara ingetoa ufafanuzi zaidi. Mjadala huu usikuzwe
bila sababu za msingi na kufunika masuala mengine muhimu ya kitaifa,”
alisema Mnyika.
Chanzo: Mwananchi