Katika
hali isiyo ya kawaida, shule moja wilayani Bagamoyo imekutwa ikiwa na
mwalimu mmoja tu anayefundisha wanafunzi kuanzia chekechea hadi darasa
la saba, wote wakifundishwa katika chumba kimoja kwa kutumia ubao
mmoja.
Hata hivyo, katika matokeo ya Darasa la Saba Mwaka huu, wanafunzi wote 12 walifaulu kuingia kidato cha kwanza.
Shule hiyo ya msingi Machala, iliyokuwa na idadi ya wanafunzi 198 na imejengwa kwa majani kuanzia chini hadi kwenye paa.
Mwandishi
wa habari hizi aliyetembelea shule hiyo, alimkuta mwalimu huyo
akiwafundisha wanafunzi hao wa madarasa tofauti wakiwa kwenye chumba
kimoja, huku ubao wa kufundishia ukiwa umechorwa mistari mitatu
kutenganisha masomo ya chekechea hadi darasa la pili, mstari mwingine
darasa la tatu hadi la tano na mwingine darasa la sita hadi la saba.
Mwalimu huyo, Christopher Rukutu, aliliambia NIPASHE Jumamosi kuwa shule hiyo hutumia kivuli cha mti kama ofisi.
Shule
hiyo iliyopo katika kijiji cha Mihunga Kata ya Miono, Wilaya ya
Bagamoyo Mkoa wa Pwani, ilianzishwa na serikali tangu mwaka 2007 ikiwa
na wanafunzi 12 ambao wamemaliza darasa la saba, mwaka huu na kubahatika
kufaulu wote.
Kwa mujibu wa mwalimu Rukutu, wanafunzi wote waliofaulu walipata alama za A na B isipokuwa mmoja aliyepata alama C.
Pamoja na kuwa katika mazingira magumu, shule hiyo kiwilaya ilishika nafasi ya sita na kimkoa nafasi ya 20.
Alisema shule hiyo haina vitabu vya kiada wala vya kufundishia na amekuwa akiazima kutoka shule za jirani.
“Ninafundisha
kwa akili za kuzaliwa sina kitabu cha mtaala wa elimu, nguvu zangu zote
nilimalizia kwa darasa la saba ili wajue kusoma, kuandika na kuhesabu.
Kwa
mwaka mzima sijafundisha darasa la nne nina wasiwasi matokeo yao
hayatakuwa mazuri kwa sababu niko peke yangu," alisema kwa masikitiko.
Alifafanua
kuwa tangu shule hiyo ianzishwe, serikali ilikuwa imewapanga walimu
wawili tu, ambao kutokana na mazingira kuwa magumu waliripoti bila
kuingia darasani na kuaga baada ya kuonyesha vyeti vya hospitali
vinavyonyesha kuwa afya zao haziwezi kustahimili mazingira magumu.
Aliilalamikia serikali kuanzia ngazi ya kata hadi wilaya kwa kuisahau shule hiyo bila kuipa msaada wowote.
Mbali
na kukosa msaada, shule hiyo pia inatumia tundu moja tu la choo kwa
wanafunzi wa kike na kiume na kusababisha wengi wao kujisaidia
vichakani.Alisema kutokana na hali hiyo, wanafunzi wengi hushambuliwa na
ugonjwa wa kichocho.
Aliiomba
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kuwapangia wanafunzi wake 12
waliofaulu katika shule yake ya Machari kwenye shule za sekondari zenye
mahitaji muhimu ili kuwapunguzia mateso wanafunzi hao.
Alisema wanafunzi wake hawajawahi kuona vitabu vya kujisomea na huduma muhimu za kiafya.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment